ASKOFU DR MUNGA ATOA SOMO KUNTU KWA VIONGOZI

Askofu Stephen Munga kushoto akisalimia na rais mstaafu Jakaya Kikwete
Anazungumuza haya Dr Munga

KUTENGENEZA HISTORIA YAKO NZURI YA KUDUMU

"Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu."
(Matayo 5:8).

Hili ni fundisho lingine zito la Yesu Kristo ambalo mara nyingine tumelichukulia juujuu. Tuanze na swali: moyo safi ni moyo wa namna gani? Moyo safi ni moyo uliotakasika ambao ndani yake hakuna hila wala unafiki. Katika "posting" yangu hapa niliwahi kuzungumzia juu ya unafiki na jinsi Yesu Kristo alivyojitenga nao na kupambana na unafiki na wanafiki. Pale nilisema kwamba hata hukumu yake ya kifo ni matokeo ya mapambano hayo. Moyo safi ni moyo uliojazwa upendo, kweli na haki. Hao waliojazwa hayo mioyoni mwao wanapewa na zawadi ya kuwa waaminifu kwa dhamiri zao katika kutetea tunu (virtues and values) hizo. Kwa hiyo wenye moyo safi ni watu ambao wanazo dhamiri safi katika kutetea upendo, kweli na haki katika maisha yao. Hao ndio watu wale ambao wanaahidiwa kumuona Mungu. Lakini je, kumuona Mungu kunamaanisha nini katika maisha yetu?

Kumuona Mungu maana yake ni kwamba kumbukumbu za watu wa jinsi hiyo zinavuka mipaka ya maisha haya. Mungu ndiye ukamilifu na utimilifu wa historia zetu. Mungu ni wa milele. Mungu anavuka mipaka ya historia ya ulimwengu tunamoishi. Kwa hiyo historia ya watu wenye moyo safi ni historia inayovuka mipaka ya maisha haya tunayoishi ulimwenguni humu. Wapo watu waliotaka kuwa mashujaa mfano wa Hitler na Idi Amin wa Uganda lakini kwa sababu hawakuwa na mioyo safi, basi historia imewatema. Hatuwakumbuki watu wa jinsi hiyo kwa mema bali tunawakumbuka kwa jinsi walivyojaribu kuubomoa ulimwengu na jamii zake. Watu wa jinsi hiyo ni wale ambao wanajitafutia utukufu wao binafsi. Kwa kuwa historia haifungwi bali ni mtiririko wa maisha kuelekea umilele, basi historia za watu wa jinsi hiyo hukatika. Historia haitakuja itokee itunze watu wa jinsi hiyo kama waliokuwa na nia ya kuujenga ulimwengu kwa mema. Walijitahidi kitumia mkono wa chuma kuumiza na kuangamiza watu na jamii zao lakini hatimaye historia iliwageuka na kuwaanika kama wasaliti wa jamii za ulimwengu.

Wakati mwingine tunapopata madaraka na mamlaka tunageuka na kujifanya miungu ya dunia. Tuanataka kila mtu atutii sisi na kuiacha njia ya kumtii Mungu wa kweli. Lakini tunafanya hayo kwa kujisahau kwamba hata sisi maisha yetu ni ya muda tu. Kila mmoja wetu anapewa nafasi ya kutengeneza historia yake chini ya mbingu. Fursa hii ya uhuru anaotupa Mungu mara nyingi tumeitumia vibaya. Tunasahau kwamba historia yetu inayodumu ni ile ambayo imesimama katika kuwa na mioyo safi iliyojengeka katika upendo, kweli na haki na kuyatunza hayo kwa dhamiri safi. Mfalme Daudi na watawala wote waliofanikiwa walitambua hivyo. Tusingekuwa tunaziimba Zaburi za Mfalme Daudi kama asingefanya hivyo. Tusingemuita Nyerere kuwa Baba wa Taifa kama asingetambua na kufanya hivyo. Hawa na wengine tunaowatambua tumeendelea kuwaheshimu ng'ambo ya vifo vyao kwa sababu walikubali kuvikwa mioyo safi. Historia zao zinabaki kwetu kwa sababu walitunza tunu za upendo, kweli na haki. Kwa maisha yao na dhamiri zao safi wamefanya mambo ambayo yalilenga katika kuhifadhi ulimwengu na jamii zake.

Mwisho niseme kwamba watawala wengi wamekuwa chambo cha dhamiri mbovu za maangamizi. Historia haijawahi kuhifadhi kumbukumbu njema kwa watu wenye roho chafu na mbaya. Kama ambavyo historia haikuwahifadhi watu wa jinsi hii ni wazi kwamba hawakufikia upeo wa juu wa historia -yaani kumuona Mungu (labda pale walipotubu) lakini hayo ni mambo ya siri ambayo hatuyatambui na kuyaweka katika historia bali tunamwachia Mungu mwenyewe. Kwa jinsi hiyo basi ili historia ikutambue na kukuweka katika historia inayovuka ng'ambo ya maisha haya ni vema kujitaabisha katika kutunza dhamiri yako inayojengwa katika upendo, kweli na haki. Hii inadai mabadiliko makubwa ya ndani. Kinyume cha hapo lazima historia itakutema hata kama unajigamba kwa majivuno makubwa. Mungu ni utimilifu wa historia za watu wote wenye mioyo safi. Tena Mungu ndiye anayeupatia ulimwengu hekima ya kufuta historia ya watu wote waletao maangamizi kwa kujifanya wao ni miungu ya ulimwengu huu.

USIJIDANGANYE. WEWE SI KITU PALE UNAPOFUATA MOYO WAKO MCHAFU!!! Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu.
EDUSPORTSTZ inakutakia maandalizi mema ya siku. inakuomba kulike facebook page yetu au kufollow kupitia blog eneo la follow by email ili kutumiwa habari kwa wakati.
Enter your email address:


Delivered by EDUSPORTSTZ
Subscribe to EDUSPORTSTZ

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post