Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amesema ikiwa atashindwa kutatua kero ya maji katika jimbo hilo hawezi kusimama na kuwaomba wananchi wamchague tena kuwa mbunge katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Bashe ametoa kauli hiyo leo Februari 12, 2018 wakati akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Clouds.
Amesema Nzega Mjini tayari miradi mbalimbali ya maji imeanza kutekelezwa na kwamba, hali ni tofauti tatizo lililopo hivi siyo kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa Ziwa Victoria ambao utawezesha kuwa na mtandao mpya wa maji wa kilomita 45 katika mji wa Nzega.
Amesema aliomba Sh460 milioni kwa Rais John Magufuli kwa ajili ya maji, kati ya hizo tayari amepatiwa Sh250 milioni.
Amebainisha kuwa fedha hizo zimetumika kufanya ukarabati wa chujio la maji na kufufua bwawa la maji la Uchami, hivyo kuwawezeaha wananchi kupata maji kwa mgawo mara mbili kwa wiki.
Pia, amesema Rais alipeleka Nzega Sh260 milioni nje ya bajeti ya halmashauri, ambazo zimetumika kujenga tangi lililopo Shule ya Msingi Nyasa na kujenga vituo vya maji katika maeneo mbalimbali ya Nzega.
Amesema miradi mingine ni ya visima 13 vinavyotumia umeme jua katika maeneo ambayo mradi wa maji wa Ziwa Victoria hautafika.
"Tunaamini miradi yote hii hadi 2020 itakuwa imekamilika, kwani mbali na hiyo nilishaomba msaada Japan wa uchimbaji wa visima sita. Kama miradi hii yote haitakamilika sina haja ya kwenda kuwaomba kura wananchi wa Nzega,” amesema Bashe.
Elimu Yetu
Post a Comment