MTIBWA SUGAR WAKIFANYA HAYA UBINGWA KWA YANGA NA SIMBA NI NDOTO YA MCHANA





ILI kufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara msimu huu, mabingwa mara mbili wa zamani, timu ya Mtibwa Sugar FC wanapaswa kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi na kuendelea kushinda michezo yao inayofanyika katika uwanja wa nyumbani (Manungu Complex, Turiani.)

Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa zamani (1999 na 2000) wameanza msimu huu vizuri wakiwa wameshinda michezo mitatu na kutoa sare mara tatu katika michezo sita ya mwanzo. Ikiwa nyuma kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa dhidi ya viongozi Simba SC kikosi hicho cha kocha Zubeiry Katwila kimeonyesha nia ya kutwaa taji msimu huu tangu walipofanya hivyo kwa mara ya mwisho miaka takribani 16 iliyopita.

Licha ya ‘kubezwa’ na kuonekana ni ‘tabia’ yao-kuanza vizuri msimu na kumaliza katika nafasi za chini mwishoni mwa msimu, upande wangu naamini Mtibwa Sugar ni timu yenye uwezo wa kushindana kwa msimu mzima na kutwaa ubingwa kama watajidhatiti katika hilo.

Kushinda pointi 35+ Manungu Complex

Kabla ya kuanza kwa msimu wa 2016/17 nilipata kuandika makala kuhusu uzembe ambao umekuwa ukifanywa na timu hiyo ya Turiani, Morogoro kiasi cha kushindwa kuonyesha upinzani hadi mwishoni mwa msimu.

Kushindwa kizembe kupata matokeo katika uwanja wa Manungu Complex dhidi ya timu ambazo wangeweza kuzifunga kuliiangusha sana timu hiyo msimu wa 2012/13 licha ya kufanikiwa kukusanya alama kumi katika michezo minne dhidi ya vigogo Yanga SC na Simba.

Unapomaliza msimu pasipo kupoteza mechi dhidi ya Yanga na Simba huku ukizishinda timu hizo mara mbili na kutoa sare mbili inamaanisha ulikuwa na kikosi kikali. Katika misimu ya karibuni Mtibwa Sugar imekuwa ikiangusha sana pointi katika uwanja wa Manungu jambo ambalo limekuwa likiwaporomosha na kwa misimu saba sasa timu hiyo imekuwa nje ya nafasi tatu za juu huku mara moja tu wakifanikiwa kumaliza msimu ndani ya nafasi nne za juu.

Kushinda michezo mitatu mfululizo katika uwanja wa Manungu Complex mbele ya timu tatu kutoka Kanda ya Ziwa (Stand United, Mwadui FC na Mbao FC) kumewafanya mabingwa hao mara mbili wa kihistoria kukusanya alama zote 9 katika uwanja wa nyumbani.

Na wakiwa wametoka kupata sare tatu mfululizo katika michezo mikubwa ya ugenini (Ruvu Shooting 1-1 Mtibwa, Yanga 0-0 Mtibwa, Simba 1-1 Mtibwa) ni wazi kikosi cha Katwila kimeonyesha mwanzo mzuri japo wengi wanachukulia ‘kuwa ni tabia yao.’ Tabia ya kuanza msimu vizuri na kumaliza vibaya.

Mchezo wao wa nne katika uwanja wa Manungu Jumamosi hii dhidi ya mabingwa mara moja wa zamani wa Tanzania, timu ya Tanzania Prisons unaweza kuanza kuonyesha picha halisi ya kile kinachotakiwa na timu hiyo kutoka mkoani Morogoro katika ligi ya msimu huu.

Katika michezo 15 ya nyumbani, Mtibwa haiwezi kupata alama zote 45 lakini wanaweza kupambana na kupata walau pointi 35 ambazo zinaweza kuwasogeza karibu na malengo ya ubingwa.

Ni lazima wapambane na kujitahidi kadri wawezavyo kushinda michezo kumi pale Manungu, sare tatu na kupoteza michezo miwili kunaweza kuwafanya kuwa juu katika msimamo siku ya mwisho ya msimu.

Pointi 20+ katika game 15 za ugenini

Si rahisi kupata alama 25 katika michezo 15 ya ugenini lakini Mtibwa Sugar ni lazima wajaribu kutafuta walau pointi 20 nje ya Manungu Complex kama kweli wanataka kurudisha ubingwa huo.

Kushinda walau michezo mitano ya ugenini kutawapa alama 15 na sare katika michezo mitano kutawapa ‘makumi mawili’ ya pointi muhimu katika game za ugenini. Wanaweza kupambana vizuri na kupata walau alama tano katika michezo mitatu ya ugenini vs Stand, Mwadui FC na Mbao FC ambazo walifanikiwa kuzifunga zote katika uwanja wa Manungu.

Kulazimisha matokeo dhidi ya timu kama Ndanda FC, Majimaji FC, Lipuli FC katika viwanja vyao vya nyumbani kunaweza kuwaongezea pointi muhimu timu hiyo yenye mseto mzuri wa wachezaji kiumri na kiuchezaji.

Naona wanaweza kupata alama zisizopungua 20 nje ya uwanja wao wa Manungu msimu huu huku tayari wakiwa wamechukua alama moja moja kwa kila mchezo kati ya game tatu za ugenini walizocheza dhidi ya Shooting na wababe Yanga na Simba. Bado pointi 17 katika michezo 12 iliyosalia ugenini kwa upande wao.

Kikosi kizuri wanacho

Golikipa mshindi mara mbili wa tuzo binafsi ya kipa bora wa VPL, Shaaban Kado, walinzi wazoefu kama Dickson Daud, Salum Kanoni, Issa Rashid, viungo wakongwe wenye ubora wakiongozwa na nahodha, Shaaban Nditti, Henry Joseph.

Hussein Javu katika safu ya mashambulizi wanaweza kuungana na vijana kama Kassian Ponela, Haroun Chanongo, Mohamed Issa ‘Banka’, Stamil Mbonde na wengineo kutengeneza timu kali ambayo inaweza kushinda ubingwa wakiweka malengo na kupambana ndani ya uwanja. Huku uwanja wa Manungu wakiutumia kwa umakini na kuugeuza ‘karata dume’ yao ya kuwapa taji la tatu la VPL.

like facebook page yetu hapa kwa habari za uhakika Propellerads

For Booking>>>



CALL>>>

Voda: +255757441463

JIUNGE NAMI KUPITIA LINK HIZI








0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post