THAMANI YA SAMATTA KUFIKIA SH 11BILION ULAYA




Samatta aliuzwa na Mazembe kwa Pauni 720,000 (Sh2 bilioni) Januari mwaka jana lakini miezi 18 tu baadaye, thamani yake hiyo imepanda maradufu.

MBWANA Samatta anaendelea kupeta tu. Ikiwa ni mwaka mmoja na nusu tu tangu auzwe na TP Mazembe kwenda KRC Genk ya Ubelgiji, thamani yake imepanda mara nne zaidi.
Samatta aliuzwa na Mazembe kwa Pauni 720,000 (Sh2 bilioni) Januari mwaka jana lakini miezi 18 tu baadaye, thamani yake hiyo imepanda maradufu.
Kwa mujibu wa mtandao wa Sofifa.com, Samatta kwa sasa ana thamani ya Pauni 4 milioni (Sh11.5 bilioni) ikiwa ni zaidi ya mara nne ya dau lake Januari mwaka jana.
Hata hivyo mtandao wa Transfermark unaotoa thamani za wachezaji duniani kote, umedai kwamba dau la Samatta kwa sasa ni Pauni 2.7 milioni (Sh7.8 bilioni).
Dau hilo la Samatta linamfanya kuwa mchezaji ghali zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka la Tanzania.

Thamani ilivyopanda
Mtandao huo wa Transfermark unaeleza kuwa dau la Samatta limekuwa likipanda kila baada ya miezi kadhaa na sasa ndiyo limefikia kiwango hicho.
Mtandao huo unasema Julai mwaka jana baada ya Samatta kucheza Genk kwa miezi sita, dau lake lilipanda kutoka Pauni 720,000 hadi Pauni 1.35.
Katika kipindi hicho, Samatta aliichezea Genk mechi 18 na kufunga mabao matano ambayo yalianza kupandisha thamani yake hiyo. Katika mechi hizo Samatta alicheza kwa dakika 905 hivyo kuwa na wastani wa bao moja kila baada ya dakika 181.
Dau la Samatta lilipanda hadi kufikia Pauni 1.98 milioni Januari mwaka huu jambo ambalo lilianza kuonyesha kuwa kiwango chake kinazidi kuimarika.
Kutokana na ushiriki wa timu yake katika michuano ya Europa Ligi, thamani ya Samatta ilipanda maradufu kati ya Januari na Machi mwaka huu hadi kufikia Pauni 2.7 milioni ambayo imetulia hapo mpaka sasa.
Hata hivyo mtandao huo wa Sofifa unadai kwamba limefikia Pauni 4 milioni na huenda likapanda maradufu kama atafanya vizuri zaidi msimu huu.

Lukaku, Neymar
Mtandao huo wa Transfermark unatoa thamani halisi za wachezaji uwanjani ambapo hadi mwezi Julai thamani ya wachezaji Romelu Lukaku na Neymar Santos zilikuwa kawaida tu tofauti na walivyouzwa.
Thamani ya Lukaku kwa mujibu wa mtandao huo ilikuwa Pauni 45 milioni lakini kutokana na mabadiliko sokoni, Manchester United ililazimika kulipa Pauni 75 milioni kumnunua kutoka Everton.
Thamani ya Neymar hadi Julai ilikuwa Pauni 90 milioni lakini PSG ililazimika kumpata kwa kulipa Pauni 198 milioni iliyokuwa imewekwa kwenye mkataba wake kama fedha ambazo zikilipwa Barcelona ingekubali kumuacha.
Hii inamaanisha kwamba hata kwa Samatta thamani yake inaweza kupanda kutokana na timu inayotaka kumnunua. Dau lake hilo linaweza kufika Pauni 10 milioni (Sh 28 bilioni).

Mabao yake
Katika hatua nyingine, Samatta anaendelea kuweka rekodi zake vizuri katika timu ya Genk baada ya kufikisha mabao 21 katika mechi 64 za mashindano aliyoichezea timu hiyo ambayo msimu huu inashiriki mashindano makubwa mawili tu.
Samatta alifunga mabao matano katika mechi 18 alizocheza msimu wake wa kwanza tu katika klabu hiyo.
Msimu uliopita alicheza mechi 29 na kufunga mabao 11 huku msimu huu akifunga mabao matatu katika mechi tano tu alizocheza.

Rekodi ya Afrika
Samatta anaendelea kutamba na rekodi kabambe aliyoiweka wakati anacheza TP Mazembe ikiwa ni pamoja na kuifungia timu hiyo mabao 20 katika mechi 40 za michuano ya Afrika.
Hiyo ni sawa na wastani wa bao moja kila baada ya mechi mbili. Katika kipindi hicho Samatta alitwaa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa pamoja na tuzo ya mchezaji Bora wa Afrika.
Samatta alishinda pia taji moja la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mazembe, mataji matano ya Ligi ya Congo, mataji matatu ya Super Cup Congo na mengine mawili ya Super Cup Afrika.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post