Diego Costa.
SAKATA la Diego Costa kugoma kurejea Chelsea bado linashika kasi na kuwa gumzo duniani kote. Straika huyo yupo nchini Brazil akiendelea kupumzika wakati wachezaji wenzake wa Chelsea wakiendelea kucheza mechi za Premier. Mhispaniola huyo mwenye asili ya Brazil, kagoma kurejea Chelsea kwa kuwa hana maelewano na kocha wake Muitaliano, Antonio Conte.
Uhusiano wake na Conte ulizorota muda mfupi baada ya msimu kuisha, kutokana na raia huyo wa Italia kumueleza kuwa hayupo kwenye mipango yake ya msimu ujao, hivyo kumtaka atafute timu. Kuanzia hapo hadi leo, Costa amegoma kufanya kazi katika kikosi cha Chelsea kilicho chini ya Conte.
Unapotazama sakata kama hili ni lazima ujiulize maswali mengi, hasa kama ukiwa ni mtu wa kutafakari mambo. Conte ameshasema Costa hayupo kwenye mipango yake na tayari ameshamleta Alvaro Morata kutoka Real Madrid kwa ajili ya kuziba pengo lake, kwa hiyo busara hapo ni kumuuza tu Costa.
Atletico Madrid inamtaka Costa, 28, kwa dau la zaidi ya pauni milioni 35 ambazo Chelsea ilizitoa ili kumnasa miaka mitatu iliyopita, lakini straika huyo pia naye anataka kutimkia klabuni hapo. Sikiliza vizuri hoja ya Costa. Anasema: “Hatima yangu tayari nilishaiamua. Lazima nirudi Atletico Madrid. Kikwazo kikubwa kinachobaki ni kwamba Chelsea haitaki kuniachia.
“Niliwaambia kwamba kama sipo kwenye mipango yao, ningependa niamue hatima yangu mwenyewe. Sitawaruhusu waamue tu ili watengeneze pesa zaidi.
Diego Costa.
“Nilipokuja Chelsea walilipa pesa kidogo kuliko ambayo Atletico wanataka kuitoa sasa. Nadhani wanapaswa kuzingatia kila nilichowafanyia. Siyo kosa langu kwamba sipo klabuni hapo. Kama lingekuwa ni suala langu ningekuwa nacheza.
“Sasa ni mwezi mzima. Mapumziko ni mazuri lakini yakizidi yanachosha.”
Unachoweza kujiuliza hapo ni kuwa kama Chelsea imeshatangaza kuwa haina mpango naye msimu huu, Atletico Madrid ipo tayari kumnunua na yeye anataka kuondoka, kwa nini basi Chelsea haitaki kumuuza?
Kama imeshaleta hadi strai ka mbadala, kwa nini haitaki kumuachia? Kwa nini inataka kumuuza kwa bei kubwa zaidi ya ilivyomnunulia wakati alitua hapo akiwa tayari ni staa, akawafanyia mambo, na sasa umri wake umesogea?
Fikiria kile ambacho Costa ameifanyia Chelsea tangu alipotua hapo mwaka 2014 kwa dau la pauni milioni 32 akitokea Atletico Madrid, halafu fikiria pia jinsi inavyotaka kuachana naye.
Nikukumbushe kidogo tu kuwa kwa misimu mitatu ambayo Costa amecheza Chelsea, mara zote amekuwa mfungaji bora klabuni hapo huku akifanikiwa kuipatia ubingwa wa Premier mara mbili (2014-15 na 2016-17).
Ninakubali kwamba Costa ana kasumba ya utukutu, ni jeuri na kiburi kwelikweli, lakini kwa kujitoa kwake huko kwa nini Chelsea isingetumia busara ya kuachana naye kwa amani?
Kuna faida gani ya kuendelea kumng’ang’ania mchezaji ambaye wamemueleza kuwa hawamtaki na kumtaka atafute timu?
Conte.
Kama walitaka aendelee kuichezea Chelsea, kwa nini sasa Conte alimtumia meseji na kumwambia hayupo kwenye mipango yake na kumtaka atafute timu?
Sasa sakata lao limefikia pabaya, kwa kuwa tayari Chelsea imeshaanza kumkata mshahara kutokana na kutokuonekana klabuni, na imetishia kuwa itakuwa ikimkata kiasi cha pauni 300,000 (zaidi ya Sh 854m) kwenye mshahara wake, kila baada ya wiki mbili asizoonekana, hatua ambayo imesababisha Costa atafute wanasheria wa kumsaidia, kwa kuwa kiburi chake ni kwamba katu hawezi kurudi kuichezea Chelsea kwa kuwa ameshaambiwa hatakiwi na atafute timu.
Wiki moja iliyopita, Costa alilalama kuwa Chelsea inamnyanyasa na inamtendea kama mnyama. Alisema: “Ninaisubiri Chelsea iniweke huru. Kwa nini hawataki niondoke kama hawanitaki?
“Uamuzi wangu ni kwenda Atletico. Nimeshazungumza na mkurugenzi wa Chelsea, Marina Granovskaia. Nilisema ‘kama kocha hanitaki, nataka niende Atletico Madrid’.
“Wanataka niende kule nifanye mazoezi na kikosi cha watoto. Sitakuwa naruhusiwa kuingia kwenye vyumba vya wachezaji wa kikosi cha kwanza na sitakuwa na mawasiliano kabisa na washkaji. Mimi siyo mhalifu! Sidhani kama ni haki kunitendea hivi baada ya yote niliyowafanyia.”
Mantiki ya kumwambia afanye mazoezi na kikosi cha kwanza ni ipi?
Najua kwamba Chelsea inataka Costa afuate utaratibu kwa kurejea klabuni, lakini kama aliambiwa atafute timu wakati akiwa mapumzikoni, arudi kufanya nini kama timu imeshapatikana? Wanachotakiwa ni kumuacha aondoke zake kwa amani tu.
Watumie busara na kutambua mchango wake na namna ya kuachana naye, waachane na kiburi chake ambacho kocha wake wa zamani, Diego Simeone ndiye anayekiweza.
Hata hivyo, Costa hataweza kuichezea Atletico mpaka mwakani, kwa kuwa klabu hiyo ina adhabu ya kutosajili hadi Januari.
Kitu ambacho kinaweza kufanyika ni kwa Costa kwenda kwa mkopo kwa Wahispaniola wengine, Deportivo La Coruna mpaka Januari.
Kingine kinachoweza kufanyika ni kujiunga na Atletico Madrid sasa lakini akae miezi michache akifanya mazoezi peke yake bila kuichezea timu hiyo hadi Januari. Hayo yote anayataka lakini siyo kubaki Chelsea.
Post a Comment