Kikosi cha Simba, kilikwenda Afrika Kusini.
KIKOSI cha Simba, kilikwenda Afrika Kusini kuweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao ambapo wikiendi hii kinatarajiwa kurejea nchini tayari kwa tamasha lao la kila mwaka la Simba Day.
Simba ilikwenda nchini humo Julai 17, mwaka huu ikiwa na wachezaji wachache kutokana na wengine kuwa na majukumu na timu ya taifa.
Baada ya kupita wiki kadhaa, kikosi chao kikakamilika huko Sauz, hali iliyowafanya benchi lao la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Joseph Omog raia wa Cameroon kuona wapi kuna upungufu ili aufanyie kazi mapema kabla ya kuanza kwa msimu.
Ikumbukwe kuwa, Simba wakiwa huko, waliendelea kufanya usajili wa wachezaji kadhaa ambapo nao walipoungana na wenzao, kikaonekana kikosi kimekamilika.
Katika wiki yao ya mwisho, wakacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Orlando Pirates na Bidvest Wits. Hizo zote zinashiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Katika mchezo wa kwanza, Simba ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Orlando Pirates, kisha mchezo uliofuata ikalazimishwa sare ya kufungana bao 1-1.
Najua wazo la kwenda kuweka kambi nje ya nchi lilikuwa na maana kubwa kwa sababu benchi la ufundi kuna kitu lilikuwa linataka kuwapa wachezaji wake, hivyo imani yangu ni kwamba wamekipata hicho kitu.
Kama tujuavyo, msimu wa 2017/18 utaanza rasmi Agosti 26, mwaka huu baada ya Agosti 23, kupigwa mchezo wa Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa kwa msimu huo utakaozikutanisha Simba na Yanga.
Wapenzi wengi wa timu ya Simba, wanasubiri kuiona timu yao ikifanya vizuri msimu ujao kutokana na kwamba wanaamini kambi ya nje ya nchi imekijenga kikosi chao vile wanavyotaka.
Kabla ya kuanza kwa msimu, watapata fursa ya kuwaona wachezaji wao kwenye mechi dhidi ya Rayon Sport katika Tamasha la Simba Day, Jumanne ijayo ya Agosti 8, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji onyesheni uwezo wenu na kuwaaminisha mashabiki wenu kwamba msimu ujao mtakuwa moto kiasi gani. Katika Simba Day, chezeni soka la uhakika. Mkifanya kinyume na hapo mtawavunja moyo wanaowasapoti.
Mbali na suala hilo la Simba, naamini kila mmoja anafahamu kwamba kesho Jumapili dirisha la usajili linatarajiwa kufungwa, hiyo ni kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambapo dirisha hilo lilifunguliwa Juni 15, mwaka huu.
Naamini kwa siku zote hizo takribani 50, kila timu imekirekebisha kikosi chake kwa ajili ya kufanya vema msimu ujao. Pia hata katika ushiriki wenu wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, mashabiki watataka kuona matunda yenu.
Nitashangaa kusikia mpaka dirisha linafungwa, timu fulani haijakamilisha usajili wake wakati kulikuwa na siku nyingi za kufanya hivyo.
TFF imekuwa taasisi ya kiungwana sana kwani ilikuwa ikitoa ukumbusho kwa klabu mbalimbali kukamilisha usajili wake ili kuepuka adhabu itakayowakumba.
Adhabu itakayoikumba timu ambayo itabainika haijakamilisha usajili wake mpaka dirisha linafungwa, itashushwa madaraja matatu. Zoezi hili la usajili ambalo linafungwa kesho linazihusisha timu za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.
Naamini hakuna timu ambayo itakubali ishushwe daraja kutokana na suala hilo. TFF nayo iwe na msimamo, kama kweli dirisha linafungwa kesho, iwe kesho kweli na isitokee siku zikaongezwa kwa maslahi ya timu fulani ambayo inaonekana ni kubwa hapa nchini.
Nasema hivyo kwa sababu kipindi kilichopita kama hiki, siku zilipoisha, ziliongezwa tena, ikatoa fursa kwa timu zilizoshindwa kukamilisha usajili wake kumalizia zoezi hilo hali ambayo haikuleta picha nzuri.
Mwisho kabisa nimalizie na Uchaguzi Mkuu wa TFF ambapo Jumamosi ya wiki ijayo ndiyo utafanyika kule Dodoma kama ilivyopangwa hapo awali.
Ni muda muafaka sasa kuanza kutega masikio na kusikiliza sera za wagombea kwani wiki ijayo ndiyo kampeni zitaanza. Hivyo tusikilize hoja za wagombea na kuzichambua vizuri, kisha achaguliwe mtu kulingana na kile ambacho tunaamini kitakuwa na manufaa kwa soka letu na wala si kwa mtu binafsi.
Tumeona uongozi uliopita jinsi ulivyoliongoza soka letu, japo kulikuwa na mabaya, lakini mazuri nayo yalikuwepo tena mengi tu. Hivyo ni jukumu la viongozi wanaokuja kuongoza kwa weledi.
Niwatakie kila la heri wagombea wote, lakini pia niwaombe wajumbe ambao watapiga kura, watuchagulie viongozi bora.
Post a Comment