Kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya amesema aliyekuwa mshambuliaji wao Ibrahim Ajibu aliyehamia Yanga, atawasumbua katika mchezo wa Ngao ya Jamii Agosti 23, mwaka huu.
Simba ikiwa bingwa wa Kombe la FA na Yanga iliyotwaa ubingwa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, zinakutana Jumatano ijayo katika mchezo wa Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ajibu msimu uliopita aliichezea Simba ambapo alikuwa mmoja wa wachezaji tishio katika kikosi hicho na kukiwezesha kushika nafasi ya pili katika ligi kuu.
Kichuya amesema uwepo wa Ajibu kwa wapinzani wao Yanga, utawasumbua katika mchezo wa Jumatano kwa kuwa wanaujua vilivyo uwezo wake.
“Ajibu ni mchezaji mzuri, hakuna asiyemjua na ni mchezaji mwenye ushindani kutokana na kiwango chake.
“Atatuletea changamoto kubwa katika mchezo huo kwani ni miongoni mwa wachezaji wenye viwango, lakini kwa upande wetu tumejipanga vizuri kuelekea mchezo huo ambao una msisimko mkubwa,” alisema Kichuya.
Simba na Yanga zote zipo Zanzibar kujiandaa na mchezo huo wa Ngao ya Jamii unaokaribisha msimu mpya wa 2017/18.
Post a Comment