Sigurdsson alifunga bao mechi yake ya kwanza aliyokuwa kwenye kikosi cha kuanza mechi Ulaya tangu Machi 2014.
Gylfi Sigurdsson alianza mechi yake ya kwanza Everton kwa kufunga bao akiwa hatua 50 kutoka kwenye goli na kusaidia vijana hao wa Ronald Koeman kufika hatua ya makundi katika ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League.
Everton walitoka sare ya 1-1 ugenini mechi hiyo dhidi ya Hajduk Split ya Croatia lakini wakasonga kwa ushindi wa jumla wa 3-1.
Klabu hiyo ya England ilikuwa ikiongoza 2-0 kutoka kwa matokeo ya mechi ya kwanza na matumaini yao yalionekana kukaribia kufutika baada ya Josip Radosevic kumbwaga kipa Jordan Pickford.
Lakini Sigurdsson, aliyekuwa akichezea Everton mara yake ya pili tangu wamnunue £45m kutoka Swansea alisawazisha sekunde 14 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili.
Bao la Sigurdsson liliwaacha Hajduk wakihitaji kufunga mabao matatu ndipo wafanikiwe kusonga.
Wayne Rooney, aliyekuwa kwenye kikosi cha kuanza mechi siku moja baada yake kutangaza kustaafu soka ya kimataifa alikuwa na fursa ya kuwapatia Everton ushindi lakini kombora lake likakombolewa na kipa Dante Stipica.
Everton watafahamu wapinzani wao hatua ya makundi droo itakapofanywa mjini Monaco Ijumaa (12:00 GMT, saa tisa alasiri Afrika Mashariki).Sigurdsson ana rekodi ya kufungia Swansea mabao mengi zaidi Ligi ya Premia, mabao 34. Aidha, anaongoza kwa kusaidia kufunga mabao mengi ligi hiyo akiwa amesaidia ufungaji wa mabao 29.
Baada ya hapo?
Everton hawatasubiri muda mrefu baada ya ushindi wao Split kurejea uwanjani, kwani watakuwa wageni wa mabingwa wa Ligi ya Premia Chelsea Jumapili alasiri (13:30 BST, saa tisa unusu alasiri Afrika Mashariki).
Post a Comment