KOCHA WA KLABU YA SIMBA, JOSEPH OMOG.
KOCHA wa klabu ya Simba, Joseph Omog, amesema uongozi wa timu hiyo umefanya jambo la maana kuipeleka timu hiyo Afrika Kusini kuweka kambi ya wiki mbili na matunda yake yataonekana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Simba ipo Afrika Kusini ikijiandaa na mechi hiyo itakayopigwa Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam pamoja na Ligi Kuu itakayoanza siku tatu baadaye.
Akizungumza na gazeti hili kutokea Johannesburg, Afrika Kusini, Omog alisema kambi hiyo itawapa nafasi ya kujiandaa vizuri kwa kuwa wapo katika mazingira tulivu.
“Kambi hii inafaida kubwa (mbili), kwanza tunaandaa timu ambayo itawapa furaha mashabiki, hatujiandai kwa sababu ya mchezo wa Yanga peke yake, lakini ni maandalizi ya mchezo huo na pili kwa ajili ya Ligi Kuu,” alisema Omog alipowasiliana na gazeti hili jana.
Aidha, alisema pia kambi hiyo itajenga msingi mzuri katika maandalizi yao ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika hapo mwakani.
Wachezaji wa Simba waliopo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ wanatarajia kuungana na wenzano mara baada ya mchezo dhidi ya Rwanda utakaochezwa Jumamosi jijini Kigali, Rwanda.
Wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Taifa Stars ni pamoja na Shiza Kichuya, Mzamir Yassin pamoja na wachezaji wapya, John Bocco, na golikipa Aishi Manula anayetajwa kusaini mkataba na klabu hiyo.
Kwa upande wa Yanga, inaendelea kujifua jijini Dar es Salaam chini ya Mzambia George Lwandamina, na tayari kocha huyo ameeleza wamemaliza mazoezi ya kujenga mwili gym na sasa wanahamia program za uwanjani
Post a Comment