MIL 30 ZAMPONZA STRAIKA YANGA



Mshambuliaji wa Yanga, Anthony Matheo (kushoto) akishangilia na Simon Msuva moja ya mechi ya Ligi zilizopita.

DAU la shilingi milioni 30 limemponza mshambuliaji wa Yanga, Anthony Matheo na kusababisha uongozi wa timu kuliweka jina lake kando huku wakiendelea na usajili wa wachezaji wengine. Matheo ni miongoni mwa wachezaji ambao mikataba yao imemalizika mwishoni mwa msimu uliopita ambapo alijiunga Yanga msimu wa 2015/16 akitokea KMKM ya Zanzibar.



Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, Yanga ilikuwa na nia kubwa ya kumwongezea mkataba Matheo lakini dau alilotaja la kuongeza mkataba ndilo lililomponza. Mtoa taarifa huyo alisema, Yanga bila kujali mchezaji huyo kutokuwa na nafasi ya kucheza katika kikosi chao walikubaliana kumuongezea mkataba kwa dau la shilingi milioni 20 lakini akakataa. “Nafikiri kila mtu anafahamu kiwango alichokuwa nacho Matheo katika timu, tulishangazwa tulipomuita kufanya naye mazungumzo, akataka asajiliwe kwa dau la shilingi milioni 30.



“Sisi tukamwambia labda tukupe shilingi milioni 20, akataka apewe ileile 30 anayotaka, hivyo tukaona ni bora tuachane naye na kumruhusu aende kutafuta maisha kwingine. “Lakini wakati tunatangaza kuachana naye, alikaa muda mrefu kidogo ndipo aliporudi na kutaka ile milioni 20 na kuomba asajiliwe, tukamwambia amechelewa tayari,” alisema bosi huyo.



Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika akizungumzia ishu hiyo ya Matheo alisema; “Usajili wetu umeshakamilika kwa asilimia 90 na tunachosubiri ni kutangaza wachezaji tuliowasajili.”

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post