Kocha wa Simba Jackson Mayanja.
SIMBA alisema kambi yake ya Afrika Kusini inaendelea vizuri na makocha wamesema itawasaidia kuwajenga wachezaji wao kuhakikisha wanakuwa fiti kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika. Simba ipo jijini Johannesburg, Afrika Kusini kwa kambi ya siku 20 ambapo watarejea nchini siku mbili kabla ya tamasha lao la Simba Day litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumamosi kutoka Afrika Kusini, Mayanja amesema kuwa, kambi yao ipo vizuri kutokana na kila mchezaji kuonyesha juhudi katika kujituma hivyo anasubiri wachezaji ambao hawajafika ili kuendelea na programu zao. Wachezaji wanaosubiriwa ni Haruna Niyonzima anayetarajiwa kujiunga na kambi hiyo baada ya kesho Jumapili ambapo atakuwa huru baada ya kumaliza mkataba na Yanga. Mchezaji mwingine anayesubiriwa ni Emmanuel Okwi ambaye sasa yupo katika majukumu ya timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes, akiichezea timu hiyo leo dhidi ya Sudan Kusini jijini Kampala.
“Kambi yetu huku ipo vizuri na tunashukuru, maandalizi yanaendelea vyema, lakini kuhusu wachezaji wetu baadhi hawajafika kwani wapo na timu zao za taifa. “Wachezaji wote wapo vizuri na wameanza kuonyesha matumaini ya kikosi chetu kitakavyokuwa msimu ujao, wanajituma na tunaendelea vizuri,” alisema Mayanja.
Wachezaji wengine wa Simba wapo na kikosi cha Taifa Stars ambacho leo kitacheza dhidi ya Rwanda kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) huko Kigali, Rwanda ikiwa ni mechi ya marudiano. Wachezaji wa Simba waliopo Taifa Stars ni Said Mohammed ‘Nduda’, Aishi Manula, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Said Ndemla, John Bocco, Mzamiru Yassin na Shiza Kichuya. Shomari Kapombe ni majeruhi yupo jijini Dar.
Post a Comment