Mshambuliaji wa Barcelona Neymar Jr akishangilia na Lionel Messi.
AWALI ilionekana ni kama kitu ambacho hakiwezekana lakini muda unavyozidi kusonga, ndivyo ambavyo mambo yanaonekana yanawezekana. Neymar kuihama Barcelona kwenda Paris Saint-Germain (PSG), sasa linaonekana linawezekana, licha ya dau la kumsajili kuwa kubwa lakini Neymar ni kama yupo tayari kwa ajili ya safari ya kuelekea Ufaransa.
Matajiri hao wa Ufaransa wanataka kuweka rekodi ya dunia kwa kumsajili Mbrazili huyo kwa pauni milioni 191. Wakati wengi wakiendelea kujiuliza juu ya maamuzi hayo ya uhamisho, hii ni tathimini ambayo inaonyesha kuwa kuna watu kadhaa nyuma ya Neymar ambao wanaweza kuchangia aondoke klabuni hapo au abaki. Neymar mwenyewe Wengine wote wanaweza kuzungumza lakini kama mwenyewe hataki kuondoka au anataka kuondoka, maamuzi yote yatategemea na kauli yake kwa kuwa Barcelona bado inamuhitaji na ni mchezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza.
Akifanya yake Uwanjani.
Inaonekana akichukua maamuzi ya kuondoka ni kutaka atwae Tuzo ya Ballon d’Or ambayo kuibeba akiwa hapo itakuwa ngumu kutokana na ufalme wa Lionel Messi ndani ya Barcelona. Messi na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid ndiyo wafalme wa soka kwa miaka kadhaa, pamoja na ubora wake wote, Neymar ameshindwa kuwafikia kwa kuwa wawili hao wana nafasi kubwa katika vikosi vyao kiutawala tofauti na yeye.
Katika timu ya taifa ya Brazil, Neymar ndiye mfalme wa timu, kila mbinu inafundishwa kumzunguka yeye wakati anapokuwa uwanjani, yawezekana hilo ndilo analolitaka litokee akiwa PSG. Baba mtu, Neymar Santos Sr Huyu ndiye wakala wa mchezaji, anasimamia mambo yote ya mikataba yanayomuhusu mwanaye.
Ndiye ambaye alifanikisha dili la usajili kutoka Santos kwenda Barcelona. Inaelezwa kuwa ameshakutana na Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona, Antero Henrique pamoja na mabosi wa PSG kwa ajili ya kujadiliana kuhusiana na suala hilo. Rais wa Barcelona, Josep Bartomeu Mamlaka yake ni makubwa klabuni, huyu akisema hamtaki mtu fulani itakuwa ngumu kubaki.
Aliwahi kunukuliwa akisema itakuwa ngumu kwa PSG kulipa dau la kumsajili Neymar, lakini inavyoonekana Wafaransa wanataka kumjibu kwa vitendo na ikiwa hivyo itakuwa ngumu kukataa biashara yenye dau nono kama hiyo. Rais wa PSG, Nasser AlKhelaifi Bosi ambaye suala la kutoa fedha siyo tatizo kwake, Mwarabu huyu amechangia kwa kiwango cha juu kuifanya timu yake kuwa na jina kubwa Ulaya kutokana na kutoa fedha nyingi za usajili. Amefanikisha kumsajili Dani Alves anayelipwa mshahara mnono kiasi cha mchezaji huyo kuikataa ofa ya kwenda Manchester City.
Rais ajaye wa Barcelona, Gerard Pique Huyu ni mchezaji lakini ana nguvu kubwa katika utawala, ameshaonyesha nia ya kutaka kuiongoza Barcelona, japo hajatamka hilo lakini huo ndiyo ukweli na ameshaanza kusoma kozi za uongozi na biashara. Klabu yake inavaa jezi zenye jina la Rakuten, huyo ni mdhamini ambaye alimpeleka yeye klabuni hapo. Ameshatamka kuwa anapenda kuona Neymar akibaki lakini ikitokea anataka kuondoka atamruhusu kwa kuwa anajua anahitaji kuwa kiongozi. Pique anakiri kuwa Neymar ni mchezaji mzuri lakini yawezekana anahitaji nguvu kubwa kikosini kwa kuwa sasa ndani ya Barca, uwanjani wenye utawala wa juu ni Messi na Luis Suarez.
Kocha wa PSG, Unai Emery Hakuwa na msimu mzuri tangu alipochukua nafasi ya Laurent Blanc, msimu mmoja uliopita, anahitaji kuiamsha tena timu yake kwa kutengeneza mipango sahihi. Akimuhitaji Neymar katika mipango yake hiyo anaweza kuwapa nguvu mabosi wake kuhakikisha usajili unafanyika. Emery alikuwa hatarini kufukuzwa kazi lakini inavyoonekana wamiliki wa klabu hiyo nao wanataka kusajili staa mkubwa kama ilivyokuwa kwa Zlatan Ibrahimovic miaka kadhaa iliyopita.
Post a Comment