DANNY AWEKA WAZI MATARAJIO YAKE YA SOKA YA BONGO




Kikosi cha singida kikendelea na mazoezi.

“NIMEPANGA
kufunga mabao 15 katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ili niweze kuwa mfungaji bora kama kule nilipotoka.” Hiyo ni kauli ya straika wa Singida United na timu ya taifa ya Rwanda, Danny Usengimana.


Straika wa Singida United na timu ya taifa ya Rwanda, Danny Usengimana akitambulishwa na Kiongozi wa Singida, Festo Sanga (kushoto).

Usengimana ambaye amejiunga na Singida United hivi karibuni kwa mkataba wa miaka miwili, kabla ya kutua Singida alikuwa akiitumikia timu ya Polisi FC ya Rwanda ambayo kwa misimu miwili mfululizo aliibuka kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda.

Msimu uliopita akiwa na timu hiyo, alifunga mabao 19 katika ligi kuu na kuibuka kuwa mfungaji bora. Singida United ambayo msimu ujao itashiriki Ligi Kuu Bara baada ya kupanda daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita, imemnyakua Mnyarwanda huyo ili kuwasaidia kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Usengimana anakuwa ni mmoja kati ya wachezaji saba wa kimataifa waliosajiliwa na timu hiyo; Wengine ni Elisha Muroiwa, Twafadzwa Kutinyu, Simbarashe Nhivi na Wisdom Mtasa (wote raia wa Zimbabwe). Shafik Batambuze raia wa Uganda na Mnyarwanda, Michel Rusheshangoga. Championi limefanya mahojiano na straika huyo anayevaa jezi namba 10 kwenye kikosi cha Singida United kinachodhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa huku kikinolewa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm akisaidiana na Jumanne Chale.

UMEJIPANGAJE KUPAMBANA NA MABEKI WA TIMU PINZANI?


Kikubwa nimejipanga vizuri kuhakikisha naifanya kazi yangu vizuri kwa ufasaha. Siogopi kupambana na beki wa aina yoyote yule.

KIPI KILICHOKULETA TANZANIA?
Ni sehemu ya kutafuta maisha, sidhani kama nitafanya kama ilivyokuwa kule nilipotoka, lakini ieleweke tu kwamba nimekuja kwa ajili ya kuifanya kazi yangu ipasavyo ili kufikia malengo niliyojiwekea ikiwemo kuibuka mfungaji bora wa ligi ya huku.

NINI TOFAUTI YA SOKA LA RWANDA NA TANZANIA?
Nimeambiwa soka la hapa lina ushabiki mkubwa lakini pia wachezaji wake wanatumia nguvu sana tofauti na kule nyumbani. Haruna Niyonzima ndiye aliyekuwa akinipa siri hizo na kunisisitiza kuwa ushindani uliopo hapa si wa kawaida na watu wanapenda sana soka. Naweza kusema hiyo ndiyo tofauti kubwa ya soka la Tanzania na Rwanda. Kikubwa amenitia nguvu ya kuja kupambana, hivyo nitajitahidi ili nifike mbali.

UMEJIPANGAJE KUISAIDIA TIMU YAKO KUWA MABINGWA MSIMU UJAO?
Nimejipanga vizuri tu sababu nimekuja kupambana kupata mafanikio, nitashirikiana vizuri na wenzangu ili kufikia malengo hayo ya kuwa mabingwa wa ligi kuu. Nadhani inawezekana.

UNAZIJUAJE SIMBA NA YANGA? Ni timu kubwa kwa hapa Tanzania, kule nyumbani Rwanda, hizo timu zinazungumzwa sana na kila mmoja anafahamu kwamba ni timu kubwa kwa hapa Tanzania, binafsi nafahamu fika ni timu nzuri na zenye ushindani.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post